Na Abdallah Nassoro-MOI
Waziri wa Afya Mhe: Mohamed Mchenjelwa ametoa wito kwa wananchi waliopoteza miguu na mikono kujitokeza kwa wingi kupata viungo bandia vinavyotolewa bure na kampuni ya Emcure Pharmaceuticals ya nchini India ikishirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa uratibu wa Ubalozi wa India nchini.
Wito huo ameutoa leo Novemba 26, 2025 katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe: Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati wa uzinduzi wa kambi maalum ya utengenezaji na ugawaji wa miguu na mikono bandia kwa wahitaji 600.
Amesema upatikanaji wa miguu hiyo bila malipo kunatoa fursa kwa wahitaji wenye kipato cha chini kufurahia maisha yako kwa kuweza kufanya kazi kama ilivyokuwa awali kabla ya upoteza kiungo husika.
“Tuhakikishe viungo vyote 600 vinapata wahitaji, wengi wamekuwa wakimudu kununua kiti mwendo kwa ajili ya kurahisisha kutembea kutokana na miguu bandia kuwa na bei kubwa ambayo hawawezi kuimudu, lakini leo hii huduma hiyo inatolewa bure hapa, kwanini basi mtu akose huduma hii” amesema Mhe: Mchenjelwa na kuongeza kuwa
“Sisi Wizara ya Afya tunaushukuru ubalozi wa India nchini kwa kuratibu jambo hili, lakini pia tunaishukuru kampuni ya Emcure Pharmaceuticals iliyotoa msaada huu, nimeambiwa viungo hivi vinatumia teknolojia ya kisasa na imara ya Jaipur, pia taasisi yetu ya MOI itumie fursa hii kujifunza teknolojia mpya ili msaada unapoisha tuweze kuendelea kuwasaidia watu wetu”
Kwa upande wake Balozi wa India Nchini Mhe: Biswadip Dey amesema msaada huo ni muendelezo wa ushirikiano mzuri ulipo baina ya Tanzania na India, ikiwa ni kambi ya pili kufanyika kwa lengo la kurejesha utu, furaha na upendo kwa waliopoteza viungo.
“Mwaka 2019 tulifanya kambi ya kwanza na mwaka huu tumerudi tena ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wetu, bila kujali gharama za vifaa hivyo sisi tunavitoa bure kwa wahitaji, naishukuru sana serikali ya Tanzania na Taasisi ya MOI kwa kuwezesha jambo hili, kwetu ni faraja kuwa sehemu ya kurejesha furaha kwa wengine” amsema Mhe: Dey
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe: Balozi Dkt. Mpoki amesisitiza kuwa huduma za uchunguzi wa awali zinazotolewa madaktari bingwa wa mifupa wa MOI ni bure, isipokuwa kwa wahitaji wanaotumia bima ya afya, bima hizo zitatumika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Emcure Pharmaceuticals iliyotoa msaada huo Bw. Satish Mehta amesema mpango uliopo kwa sasa ni kuleta huduma jongefu za karakana za utengenezaji wa viungo bandia ili uwafikia wahitaji walio pembezeno mwa nchi.
“Ninatarajia kuleta karakana jongefu ili kuwezesha kuwafikia watu wengi wenye uhitaji maeneo ya vijijini na hii itawapunguzia gharama za kusafiri kufika hapa kufuata huduma, ninafurahi kuwa sehemu ya watu wanaorejesha furaha kwa jamii ya Watanzania” amsema Mehta
Kwa upande wake mmoja wa wanufaika kwa viungo hivyo bandia Bw. Amir Bakari ameishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa msaada huo pamoja na taasisi ya MOI na ubalozi wa India nchini.