waziri simbachawene aipongeza MOI kwa huduma bora

Na Erick Dilli-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb) ameipongeza Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hizo leo Juni 17, 2025 katika Viwanja vya Chinangali Park, Jijini Dodoma, wakati alipotembelea banda la MOI na kuelezea namna huduma zilivyokuwa bora na kutoa ushuhuda wa huduma za taasisi hiyo.

“Mimi ni shuhuda mkubwa wa huduma zenu kwani nilikuwa na mdogo wangu ambaye pingili ya 6 na 7 zilihama lakini baada ya kuja kwenu (MOI) kupata matibabu sasa hivi anaendelea vizuri” amesema Mhe. Simbachawene na kuongezea

“Kwa sasa huduma zenu zipo vizuri sana, niwapongeze kwa kazi mnayoifanya sasa wagonjwa wetu wenye shida za mifupa wanatibiwa hapahapa nchini… Hakuna haja tena ya kwenda nje ya nchi na hii yote imetokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita”

Kwa upande wake, Daktari Bingwa Mbobezi wa Mifupa MOI Dkt. Tumaini Minja amemuelezea Mhe. Simbachawene namna taasisi imeweza kuzijengea uwezo huduma zake za kibingwa na kibobezi kwa hospitali za kanda na rufaa.

“Tumezijengea uwezo hospitali za rufaa na kanda ambapo madaktari wa hospitali wameweza kutoa huduma za mifupa kwa wagonjwa, hii yote ni katika kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi” amesema Dkt. Minja

Amezitaja baadhi ya hospitali hizo kuwa ni Nyangao (Lindi), Hospitali ya Kanda ya kusini Mtwara, Hospitali ya rufaa Ndanda, Hospitali ya rufaa ya Nkinga, Hospitali ya Mnazi Mmoja (Zanzinzar) na Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro.

About the Author

You may also like these