Waziri kikwete aongoza watumishi wa afya kuaga mwili wa Dkt. Mango

Na Amani Nsello- MOI

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) leo Mei, 31, 2025 amewaongoza mamia ya Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), JKCI, MNH, MUHAS na waombolezaji wengine kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Dkt. Mechris Mango aliyekuwa Daktari Bingwa wa Radiolojia na Meneja wa Idara ya Uchunguzi wa taasisi hiyo.

Tukio hilo limefanyika katika eneo la kusubiria huduma, MOI Clients’ Lounge ambapo viongozi mbalimbali wakiemo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Mpoki Ulisubisya, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mtendaji wa MNH Dkt. Rachel Mhaville, Mkurugenzi Mtendaji wa TMDA Dkt. Adam Fimbo, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu NHIF Dkt. David Mwenesano watumishi wa MOI, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wafika kutoa heshima zao za mwisho.

Akitoa salamu za rambirambi Mhe. Ridhiwani Kikwete alimwelezea Dkt. Mango kuwa alikuwa mtu aliyejitoa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kwamba kiburi, maringo na majivuno kwake hakuvipa nafasi.

“Dkt. Mango alikuwa msaada mkubwa kwa familia yangu, hata kwa wananchi wangu wa Jimbo la Chalinze… Walipopata ajali nilimtafuta Dkt. Mango na aliwasaidia, muda mwingi aliutumia kuwa hapa MOI kuwahudumia wagonjwa” amesema Mhe. Kikwete

“Alikuwa mtu ambaye unaweza kumpigia simu muda wowote na kuwa tayari kutoa msaada, alijitoa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi” amesisitiza Mhe. Kikwete

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amewashukuru Waombolezaji wote waliofika katika taasisi hiyo na kutoa heshima za mwisho kwa Dkt. Mango na kuwaomba watu hao kuyaishi yale mema yote ya marehemu huyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakata Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema taasisi yake inatoa pole kwa MOI, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo na kwamba watamkumbuka marehemu kwa umahiri wake katika taaluma ya radiolojia.

Aidha ,Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH) Dkt. Rachel Mhaville amesema wanaungana na wadau kutoa salamu za rambirambi na kwamba tasinia ya utabibu imepoteza miongni mwa watu muhimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Laurence Museru amesema marehemu Dkt. Mango ameacha alama kwa utendaji kazi wake mahiri na kwamba tasnia hiyo itaendelea kumkumbuka.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu MOI, Bw. Orest Mushi amesema kuwa Dkt. Mango alizaliwa Julai 19, 1976 katika Hospitali ya Ocean Road ya Jijini Daar es Salaam na aliajiriwa MOI Februari 2005, kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka Dkt. Mango alipandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Idara ya Uchunguzi hadi umauti wake ulipomkuta Mei 28, 2025 Hospitali ya Mzena iliyopo Jijini Dar es Salaam

Awali Mchungaji Baraka Butoke kutoka Kanisa la Adiventista Wasabato akiongoza Ibada maalum ya kutoa heshima za mwisho kwa Dkt. Mango amewaasa walio hai kutengeneza mahusiano mazuri na Mungu huku akiwambia kwamba kifo ni halisi na sio hisia na kifo hakijali wala hakiogopi mtu na hatma ya binadamu anayo Mwenyezi Mungu pekee.

“Kifo ni halisi, sio falsafa, kifo ni haki ya kila mmoja wetu, uwe mwema uwe mbaya, uwe tajiri uwe masikini, siku ikifik utakuna nacho, basi jenga mahusiano mema na Mungu uwe na mwisho mwema” amesema Mchungaji Butoke.

Marehemu Dkt. Mango anatarajiwa kupumuzishwa katika nyumba yake ya milele kesho Juni, 01, 2025 katika makaburi ya Kondo, Ununio jijini Dar es Salaam.

About the Author

You may also like these