Wazee 608 wapatiwa matibabu ya kibingwa kutoka MOI kwenye kambi maalum mnazi mmoja, Dar es salaam

Na Amani Nsello – Dar es Salaam

Zaidi ya wazee 600 wamepatiwa matibabu ya kibingwa na kibobezi kutoka kwa Wataalam wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), kupitia kambi maalum ya utoaji huduma za afya iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 16 hadi Oktoba 18, 2025.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 daktari kutoka idara ya upasuaji wa ubongo, Dkt. Manase Ng’wenzi amesema kuwa huduma zilizotolewa ni pamoja na uchunguzi wa matatizo ya mifupa, viungo, mgongo, ushauri wa tiba lishe, mazoezi tiba, maonesho ya viungo bandia pamoja na ushauri wa kitaalamu kwa wagonjwa wenye matatizo ya muda mrefu.

“Wazee wengi hupata changamoto ya kutopata huduma za kibingwa kwa ukaribu. Kupitia kambi hii, tumeweza kuwahudumia zaidi ya wazee 600 kwa siku tatu, ambapo baadhi yao wamepewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya kina zaidi MOI,” alisema Dkt. Manase.

Kwa upande wake, Bi. Zaituni Ramadhani, mmoja wa wazee waliopatiwa matibabu katika kambi hiyo, ameishukuru MOI kwa kupeleka huduma hizo karibu na wananchi.

“Nimefurahi sana. Sikuwa na uwezo wa kwenda MOI mwenyewe, lakini leo nimepata matibabu hapa karibu… Nawashukuru madaktari wote na serikali kwa kutukumbuka sisi wazee,” amesema Bi. Zaituni

Kambi hiyo imeandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya MOI ikiwa ni mkakati wa serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi hasa makundi maalum kama wazee.

About the Author

You may also like these