Wauguzi MOI wakumbushwa kuzingatia maadili ya kazi

Na Amani Nsello- MOI

Katika kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani, wauguzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamekumbushwa kuendelea kuzingatia maadili, huruma na mshikamano wakati wa kuwahudumia wagonjwa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, leo Jumatano Juni 4, 2025, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MOI, Bw. Fidelis Minja amewasisitiza wauguzi kuendelea kuwa na maadili mema na kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea.

“Taaluma ya uuguzi inategemea zaidi maadili, tunapaswa kumtanguliza mgonjwa mbele ya yote na kufanya kazi kwa huruma, uadilifu na moyo wa kujitolea” amesema Bw. Minja na kuongezea

“Ni muhimu sisi wauguzi kuwa kitu kimoja… Umoja wetu ndio nguvu ya mafanikio katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.”

Katika kuenzi siku hiyo, wauguzi hao wamefanya tendo la huruma kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi waliolazwa hospitalini hapo.

Zoezi hilo limeongozwa na Said Mwanemo, Kiongozi wa wauguzi katika Idara ya Dharura.

“Tuliona umuhimu wa kuadhimisha siku hii kwa vitendo, tumewaletea watoto hawa msaada kama ishara ya upendo, kujali na mshikamano wetu kama wauguzi.” amesema Mwanemo

Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Bw. John George amewashukuru wauguzi hao kwa moyo wao wa upendo kwa kuwapa msaada na kuwasihi kuendelea kutoa msaada wa aina hiyo.

About the Author

You may also like these