Wauguzi MOI wahimizwa kutoa huduma bora kwa wateja

Na Amani Nsello- MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma zake kwa kutoa mafunzo mahsusi kwa wauguzi wake yakilenga kuboresha namna wanavyowahudumia wagonjwa na wateja kwa ujumla.

Katika mafunzo hayo wauguzi hao wamefundishwa umuhimu wa kutoa huduma kwa ukarimu, kuwapokea wagonjwa kwa huruma na ‘kuvaa viatu vya mteja’ ili kuelewa hisia, mahitaji na changamoto wanazopitia wagonjwa.

Akizungumza leo Alhamis Desemba 04, 2025 Bw. Jumaa Almasi Meneja Ustawi wa Jamii na Tiba Lishe wa MOI amesisitiza umuhimu wa kubadili fikra na mtazamo wa utoaji wa huduma.

“Ni muhimu kila mgonjwa anayekuja hapa (MOI) ahisi kuthaminiwa, hivyo mafunzo haya yanatupa nafasi ya kujipanga upya, kuboresha mawasiliano yetu na wagonjwa na kuhakikisha tunatoa huduma zenye utu na zinazozingatia viwango bora vya kitaaluma” amesema Bw. Almasi

Pia, Bw. Almasi amewaambia wauguzi hao kuzingatia mila na desturi za kila mgonjwa anayefika katika taasisi hiyo na kuzielewa hisia za wateja.

Kwa upande wake, Meneja Wagonjwa wa Ndani wa MOI Bi. Magreth Kumpuni, amewaasa wauguzi hao kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na kuyatafsiri moja kwa moja katika utendaji kazi wa kila siku.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma yenye ustaarabu na kuifanya MOI kuendelea kuwa taasisi inayoaminiwa na wananchi kwa kutoa huduma bora.

About the Author

You may also like these