watumishi wapongezwa kwa kuboresha huduma, waaswa kuwa wabunifu kukataa rushwa

Na Abdallah Nassoro-MBWENI

Wafanyakazi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamepongezwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kuboresha hali ya utoaji huduma huku wakiaswa kuendelea kuwa wabunifu katika kutoa huduma kwa wananchi ili waweze kupona haraka na kuendelea kukataa rushwa ambayo ni adui wa haki.

Pongezi hizo zimetolewa leo Oktoba 3, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Prof. Charles Mkony katika kikao cha tano cha baraza la tano la wafanyakazi wa MOI kinachoendelea ukumbi wa APC uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.

“Nafahamu kazi nzuri mnayofanya , hongereni kwa kuongeza bidii katika kuwahudumia wananchi… ni lazima jamii ifahamu kuwa MOI inatoa matibabu ya kipekee kabisa tofauati na maeneo mengine, huduma zake ni za kipekee na zinahitaji ubunifu zaidi ili kuwawezesha wagonjwa kupona haraka” amesema Prof. Mkony na kuongeza

“Wakati menejimenti wakiendelea na uboreshaji wa maslahi ya watumishi na miundombinu ya kufanyia kazi, niwaombe watumishi endeleeni kuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa, sijasikia kwa siku za hivi karibuni na ndiyo maana nasema endeleeni hivyo”

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amewapongeza watumishi wa MOI kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwata kuendelea na ari hiyo ili wananchi waendelee kufurahia huduma bora.

“Naomba niwapongeze watumishi wote wa MOI kwa kuboresha hali ya utoaji huduma, hata malalamiko kutoka kwa wateja wetu yamepungua, hii ni ishara kuwa tumeongeza uwajibikaji katika majukumu yetu” amesema Dkt. Lemeri na kufafanua kuwa

“Watumishi wetu kwa ujumla wake, tumefanikiwa kutekeleza majukumu yetu kwa asilimia 92 ndani ya miezi Minane kuanzia Januari hadi Agosti 2024…tumefanikiwa kuanzisha huduma mpya 17, upatikanaji wa dawa umepanda kutoka asilimia 96 hadi 98”

Aidha amesisitiza kuwa wafanyakazi hao wameweza kufikia asilimia 84 ya utekelezaji wa mpango makakati wa taasisi katika kuongeza kasi ya utoaji huduma bora kwa wananchi.

About the Author

You may also like these