Watumishi MOI wanolewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza

Na Amani Nsello- MOI

Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamepewa elimu maalum kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu, kisukari, saratani, Ukimwi (VVU) na magonjwa ya moyo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuboresha afya na ustawi wa watumishi wake.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Alhamis Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa MOI, Bw. Orest Mushi, amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu kinga na udhibiti wa magonjwa hayo ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi nchini.

“Watumishi wetu ni rasilimali muhimu sana. Ili waweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa, ni lazima na wao wawe na afya njema. Mafunzo haya yatawasaidia kujitambua kiafya, kubadili mtindo wa maisha na kupunguza hatari ya kuugua magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Bw. Mushi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Bw. Fidelis Minja, ameeleza kuwa taasisi hiyo imeweka mkakati endelevu wa kuhakikisha elimu ya afya kwa watumishi inatolewa mara kwa mara.

“Tumeamua kuwekeza kwenye elimu ya kinga. Afya ya mtoa huduma ni msingi wa ubora wa huduma kwa mgonjwa. Tunataka kila mtumishi wa MOI awe balozi wa afya bora, si kazini tu bali hata katika jamii zao,” amesema Bw. Minja.

Naye, Meneja wa Ustawi wa Jamii wa MOI, Bw. Jumaa Almas, amesisitiza kuwa afya ya akili na ustawi wa watumishi ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo amebainisha kuwa mazoezi, lishe bora na ushauri wa kisaikolojia ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele.

Kwa ujumla, elimu hiyo imetajwa kuwa chachu ya kujenga nguvu kazi yenye afya bora, yenye tija, na inayoweza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wanaofika MOI kila siku.

About the Author

You may also like these