watumishi MOI wanolewa kuhusu e-mrejesho

Na Abdallah Nassoro-MOI

Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamehudhuria mafunzo ya siku mbili ya mfumo wa kidigitali wa E-mjeresho ili kuwezesha kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, maoni ushauri na pongezi kutoka kwa wateja wao.

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa MOI, Orest Mushi amesema wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo siku ya Jumatano Novemba 06, 2024 katika ukumbi wa hospitali ya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuboresha huduma.

“Mafunzo haya ni muhimu kwetu kwasababu yanakwenda kuongeza wigo wa wetu wateja kutoa mrejesho wa huduma zetu…kwa kupata mrejesho wa huduma zetu tunaongezewa fursa ya kufanya maboresho zaidi” amesema Mushi

Kwa upande wake Meneja Usimamizi Ubora wa Shirika la Usimamizi na Maendeleo ya Afya (MDH) Dkt. Hellen Sirili amesema matumizi ya E-mrejesho yatasaidia wananchi kushiriki katika kuboresha huduma za taasisi.

“Ni muhimu jamii ishiriki uboresha huduma katika taasisi, njia sahihi ya wao kushiriki ni kufungua milango la kupokea mrejesho, kwahiyo E-mrejesho inakuja kuwasaidia kujitathimini” amesema Dkt. Sirili

Kwa upande wake Meneja Udhibiti Ubora wa MOI Dkt. Paul Kazungu amesema mafunzo hayo yatasaidia MOI kufanikisha adhima yake ya kuhakikisha wateja wake wanaridhika na huduma wanazopata.

“Tunataka mteja akifika MOI aweze kupokewa na mtoa huduma yeyote na kupata maelekezo sahihi ya mahitaji yake sio lazima aende kwa mtoa huduma kwa wateja ili awezekuelekezwa” amesema Dkt. Kazungu

About the Author

You may also like these