Watumishi MOI wajitokeza kupima magonjwa yasiyoambukiza

Na Amani Nsello- MOI

Katika muendelezo wa Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs), watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamejitokeza kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu.

Akizungumza jana Novemba 18, 2025, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Magonjwa ya ndani na huduma za Dawa wa MOI, Dkt. Deodata Matiko, amesema mwitikio wa watumishi umekuwa mkubwa na unaonyesha uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

“Muitikio ni mkubwa sana, watumishi wamejitokeza kwa wingi kupima. Natoa wito kwa watumishi wengine waendelee kujitokeza kupima na kujua afya zao, kwani hatua ya kwanza ya kujikinga ni kujua afya yako,” amesema Dkt. Deodata.

Amezitaja huduma zinazotolewa kuwa ni pamoja na kupima kisukari, shinikizo la damu, urefu, uzito pamoja na ushauri wa tiba lishe na afya ya akili.

Kwa upande wake, mmoja wa watumishi wamejitokeza kupima, Hilali Athuman, alisema zoezi hilo limekuwa msaada mkubwa kwao, kwani wengi hupata changamoto ya kutopata muda wa kufuatilia vipimo muhimu vya afya.

“Nimefarijika sana kupata huduma hizi kazini. Nilipima shinikizo la damu na sukari, na nimepata ushauri wa lishe ambao sijawahi kupata hapo awali. Nawaomba watumishi wenzangu wajitokeze, kwani afya ni mtaji,” amesema Hilali

Wiki ya Kujikinga na Magonjwa Yasioambukiza inalenga kuongeza uelewa na kuhimiza hatua za kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi nchini.

About the Author

You may also like these