Na Abdallah Nassoro-MOI
Watumishi wa Kitengo cha Utafiti, Mafunzo na Ushauri katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wanapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya matumizi ya nyenzo mpya za ukusanyaji, uchakataji na uchambuzi wa taarifa za kitababu ili kuboresha hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Oktoba, 22, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa jengo jipya na kufunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe: Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ambaye amewahimiza watumishi hao kuzingatia usahihi wa taarifa wanazokusanya ili ziweze kutoa majibu ya changamoto za wagonjwa na taasisi.
“Maswali yote tuliyonayo katika taasisi yetu lazima yajibiwe na takwimu…na ni lazima takwimu hizo ziwe sahihi…ukiwa na taarifa sahihi itawezesha pia madaktari kuweza kumfuatilia maendeleo ya mgonjwa akiwa nyumbani kwake” amesema Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa
“Usahihi wa takwimu zetu ni jambo muhimu sana, tumejiwekea lengo la kuchapisha machapisho ya kitabibu 20 kwa mwaka, ili machapisho hayo yaweze kuwa na athari chanya kwa matumizi ya kutatua changamoto zetu usahihi wa takwimu ni nyenzo muhimbi, ifike mahala takwimu ndiyo ziongee”
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kitengo cha Utafiti, Mafunzo na Ushauri Dkt. Joel Bwemelo amesema mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia mbinu za kisasa katika kukusanya, kuchakata na kuchambua taarifa za kitabibu.
“Usahihi wa taarifa ni jambo muhimu sana ili kufikia lengo la kuchapisha taarifa zenye ubora, mafunzo haya yanalenga pia kuwajengea uwezo kutumia nyenzo mpya za kukusanya, kuchakata na kuchambua taarifa hizo” amesema Dkt. Bwemelo
Amefafanua kuwa “Katika mafunzo haya hatuangalii tu usahihi wa taarifa, lakini pia utimilifu na ujumuishi wa taarifa hizo ili kuvutia tafiti kubwa zitakazojikita katika kuangalia changamoto za wagonjwa wetu na kupata majibu sahihi ya kitabibu”