Watalaam bobezi kutoka Ireland watua MOI kutoa matibabu ya mifupa kwa watoto

Na Mwandishi wetu- MOI

Jopo la madaktari bingwa bobezi wa mifupa, ganzi na wauguzi kutoka Ireland kwa kushirikiana na wenzao kutoka Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wanaendesha kambi maalum ya siku nne ya matibabu ya mifupa kwa watoto.

Mapokezi ya jopo hilo yamefanyika leo Octoba 20, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ambapo amesema kambi hiyo itafanyika kuanzia leo tarehe 20 hadi tarehe 24 oktoba, 2025 kwa lengo la kutoa matibabu ya watoto wenye miguu iliyopinda, miguu mifupi, matege na mivunjiko ya mifupa.

“Leo tumepokea jopo la madaktari bingwa bobezi wa mifupa, daktari bingwa wa ganzi na wauguzi kutoka hospitali ya Children`s health Ireland iliyopo Dublin, ambao wanatoa matibabu ya mifupa kwa watoto wenye miguu mifupi, kunyoosha miguu iliyopinda, matege na mivunjiko ya mifupa kwa siku tano kwa kushirikiana na timu ya wataalam wa hapa MOI” amesema Dkt. Mpoki

Dkt. Mpoki amesema Taasisi ya MOI imekuwa ikishirikiana na hospitali hiyo kwa zaidi ya miaka minne kwa kuendesha kambi mbalimbali za matibabu ambapo wamefanikiwa kuondoa rufaa za wagonjwa hao za kufuata matibabu hayo nje ya nchi.

Aidha, Dkt. Mpoki amesema Taasisi ya MOI inatarajia kuanzisha tiba mtandao (Telemedicine link) ili kuwaunganisha wagonjwa na madaktari bingwa na bobezi kwa kutoa tiba kwa njia ya mtandao bila kusafiri umbali mrefu.

Kwa upande Daktari bingwa bobezi wa mifupa kwa watoto kutoka Ireland, Dkt.Paula Kelly amesema kupitia kambi hizo wamekuwa wakijengeana uwezo na wenzao kutoka MOI katika kuhakikisha wanazidi kutoa matibabu ya kibingwa bobezi kwa watoto wenye matatizo hayo ya mifupa.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha matibabu ya Mifupa kwa watoto kutoka MOI, Dkt. Bryson Mcharo amesema leo wanawafanyia uchunguzi wagonjwa wote wenye matatizo hayo na wale watakao onekana wanahitaji matibabu zaidi watafanyiwa upasuaji .

Ameongeza kuwa katika kambi hiyo watatumia kifaa cha kisasa cha Taillor Spartial Frame (TSF) kunyoosha miguu ya wototo iliyopinda na kinasaidia kutoa kipimo halisi cha urefushaji wa miguu mifupi.

About the Author

You may also like these