Na Abdallah Nassoro – Mnazi Mmoja
Wagonjwa 783 wamefaidika na huduma za matibabu ya kibingwa na bobezi zilizotolewa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika wiki ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja wa Magonjwa ya Ndani na huduma za Dawa wa MOI Dkt. Deodata Matiko amebainisha hayo wakati wa ufungaji wa maadhimisho Novemba 15, 2025.
Dkt. Deodata amebainisha kuwa wagonjwa hao walifaidika na huduma za vipimo vya awali bila malipo, kuonana na madaktari bingwa, bobezi, elimu ya lishe, mazoezi tiba na viungo saidizi.
“Muitikio ulikuwa mkubwa sana, hadi leo tunahitisha kambi hii wagonjwa 783 wamepatiwa matibabu, wapo tuliowapa rufaa ya kuja MOI kuendelea na matibabu zaidi, wapo waliopata elimu na ushauri katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza” amesema Dkt. Deodata
Ameongeza kuwa “Baada ya kukamilisha kambi ya wananchi, Novemba 18, 2025 tutatoa matibabu kama hayo kwa watumishi wa MOI na ndugu wa wagonjwa waliopo pale”
Amesema katika utoaji wa huduma hiyo bima za afya zitatumika kwa watumishi na huduma za vipimo vya awali bila malipo kwa wasio na bima ya afya.
“Lengo ni kuhalikisha huduma hii inawafilia si wananchi pekee bali kwa watumishi kwakuwa magonjwa haya hayachagui mtu…huduma kwa upande wa MOI zitatolewa hadi Ijumaa Novemba 21,2025” amefafanua