Wagonjwa 1,082 wanufaika na kliniki ya MOI chato

Na Erick Dilli- Chato

zaidi ya wagonjwa 1,082 wanufaika na kliniki ya huduma za Kibingwa na kibobezi za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu kutoka MOI katika hospitali ya kanda ya rufaa Chato.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 19, 2025 katika ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya katika Hospitali ya rufaa ya kanda Chato (CZRH).

DKt. Mpoki amesema Taasisi ya MOI itaendelea kusogeza huduma zake za kibingwa na kibobezi za mifupa, Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu katika hospitali ya kanda Chato na hospitali nyingine ili kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

“Taasisi ya MOI itaendelea kutoa ushirikiano na Hospitali ya kanda ya Chato ili kuhakikisha wagonjwa kutoka mkoa wa Geita wenye changamoto ya Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu wanahudumiwa huku huku bila kulazimika kuja Dar es Salaam” amesema Dkt. Mpoki na kuongozea

“Kwa kufanya hivyo tutasaidia kuokoa gharama na usumbufu kwa wagonjwa kwenda umbali mrefu kupata huduma ambazo zinatolewa MOI”

Akimpokea Dkt. Mpoki, kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya kanda ya Chato Dkt. Oswald Lyapa ameeleza idadi hiyo imepatikana kuanzia Novemba 2024 Mpaka Septemba 2025 na wagonjwa wengi kutoka ukanda huu na mikoa jirani wanazidi kunufaika kupitia kliniki hii.

Daktari kutoka kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Kanda Chato Dkt. Jackson Fulani amefanunua kuwa Kati ya wagonjwa 1,082 wagonjwa 722 walikuwa ni wa Mifupa na 360 ni wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu

MOI itaendelea kujengea uwezo Hospitali za Mikoa katika utoaji wa Huduma za Kibingwa za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu ili kuhakikisha huduma za kibingwa zinasigezwa karibu na wananchi

About the Author

You may also like these