wadau mbalimbali waendelea kujitokeza kutoa msaada kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi MOI

Na Abdallah Nassoro-MOI

Wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza kutoa msaada kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI)

Siku ya Septemba 28, 2024 Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kutoka Parokia ya Mtakatifu Kizito Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam wamewatembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto waliolazwa na wanaondelea kupatiwa matibabu katika taasisi ya MOI.

Akikakabidhi msaada huo Mwenyekiti WAWATA Parokia ya Mtakatifu Kizito-Kilongawima Mbezi Beach Florence Nyange amesema kuwa wao kama waumini Wakatoliki wanawake wametumia siku ya WAWATA (WAWATA DAY) ili kutoa msaada kwa ajili ya mahitaji ya watoto hao, ambapo wametoa dawa za binadamu (kulingana na uhitaji wao), taulo (pampers) na maziwa.

“Tungeweza kula na kunywa katika siku yetu ya WAWATA (WAWATA DAY) lakini tukasema hapana, tukawaone watoto na tutoe msaada, tumeleta madawa kulingana na risiti tuliyokuwa tumepewa, pampers, maziwa hicho ndo tulichojaaliwa kukusanya kutoka kwa wamama wenzetu”. Amesema Bi Florence

Bi. Florence ameongeza kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kusaidiana na serikali kutoa matibabu kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.

Pia umoja huo umelipia gharama za upasuaji kwa mtoto mmoja mwenye tatizo la kichwa kikubwa.

Awali akiwakaribisha wanawake hao Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa MOI, Teofrida Mbilinyi ametoa rai kwa asasi na taasisi nyingine kujitokeza kutoa misaada kwa watoto hao kwa sababu baadhi ya jamii huwatenga, hivyo wakiwashika mkono inawasaidia kurudisha furaha yao na matumaini ya kuishi.

About the Author

You may also like these