Viongozi na Watumishi MOI wapewa mafunzo ya kusimamia ubora wa huduma za tiba kwa wagonjwa na kuzingatia maadili ya taaluma.

Na Mwandishi Wetu-MOI

Viongozi wa Kurugenzi, Idara na Vitengo wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamekumbushwa kuhakikisha wanasimamia vema suala la ubora wa huduma kwa watendaji wa chini yao ili kauli mbiu ya MOI mpya iweze kuakisi uhalisia.

Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Oktoba, 27, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi katika kikao cha pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi hiyo chenye lengo la kutathimini hali ya utoaji huduma katika taasisi hiyo.

Prof. Makubi amesema ni jukumu la kila msimamizi kuhakikisha walio chini yake wanafuata amaadili, umahili/weledi wa taaluma zao na kuzingatia kanuni (SOPs) za utoaji wa huduma bora kwa wateja ili kuendelea kuboresha hali ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Aidha Mkurugenzi huyo aliwaomba baadhi ya watumishi kuacha mara moja tabia ya kushawishi wagonjwa waliofika MOI kwenda mitaani.
“Baadhi yenu wachache, msiwashawishi wagonjwa kuhama hospitali kama wameshafika MOI, ninyi si madalali, menejimenti haipo tayari kuona wagonjwa wanaokuja hapa kwa jina la MOI wanahamishwa kwenda kwingine ” amesema Prof. Makubi

Akitoa wasilisho lake Mwanasheria wa MOI, Selemani Mgerwa amesema ni muhimu kwa watoa huduma kuzingatia Maadili, viapo, uzalendo kanuni na sheria za kazi ili kutoa huduma zenye ubora unaokubalika na kuepuka kuchafua hadhi za watumishi , Taasisi na Serikali.

Kwa upande wake Mtaalam wa Huduma bora kwa wateja Padre John Kasembo amesema pamoja na mazingira magumu wanayopitia wakati wa utoaji wa huduma, watumishi wa MOI hawana budi kuwa tayari kujitoa sadaka kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

“Kuweni tayari kubadilika na kujitoa sadaka ili wengine wafaidike na huduma yako, nataka niwaambie kuwa huduma bora kwa wateja ndiyo uchawi wenyewe katika huduma/biashara, jiulize ukifa ni nani atalia, acheni nyayo huku mkiomba Mungu awasaidie katika utume wenu” amesema Padre Kasembo.

About the Author

You may also like these