Na Erick Dilli- MOI
Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Fhamaz Trust kutoka nchini Uingereza imeahidi kuchangia mashine mbili maalum za kuzalisha joto kwenye chumba cha upasuaji katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili MOI.
Hayo yamesemwa Julai 18, 2025 na Bi. Zarnat Datoo ambaye ameambatana na mumewe ambaye pia mmiliki mwenza wa taasisi hiyo, amesema ahadi hiyo ya kuchangia mashine hizo imekuja baada ya kutembelea chumba cha upasuaji MOI.
“Kwa moyo wa amani na upendo tumeona ni vyema kuzidi kuweka alama pale ambapo mgonjwa anakuwa na furaha baada ya kufanyiwa upasuaji haswa kwa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi” amesema Bi. Zarnat na kuongezea
“Tunaahidi kuongezea mashine hii ya kumpa mgonjwa joto wakati wa upasuaji pamoja na mashine ya kupasha joto maji au damu zinazotumika wakati wa upasuaji kwa lengo la kuwa sehemu katika kufanyikisha matibabu ya wagonjwa”
Kwa upande wake, Muuguzi Mbobezi kutoka chumba cha upasuaji MOI, Bw. Juma Rehani ameishukuru taasisi hiyo kwa kuzidi kuweka alama MOI haswa kwenye matibabu ya watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi kuanzia gharama za upasuaji na huduma nyinginezo.