T Group waunga mkono jitihada za MOI kuhudumia wagonjwa.

Na Erick Dilli- MOI

Kikundi cha T Group waunga mkono jitihada za utoaji huduma za afya katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kukabidhi msaada wa mashine 10 za kupimia shinikizo la damu.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Septemba 6, 2025, ambapo Kiongozi wa Wodi 4B, Bi. Sada Mbilinyi, akimwakilisha Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, alipokea vifaa hivyo na kulishukuru kundi hilo kwa moyo wao wa kujitoa.

“Tunashukuru kwa kutoa huu wa mashine hizi za kupima shinikizo la damu kwani itasaidia kuongeza ufanisi na viwango vya utoaji huduma kwa wagonjwa wetu hapa MOI,” alisema Bi. Mbilinyi.

Akizungumza kwa niaba ya T Group, Mwenyekiti Bw. Martin Ngonyani alisema mbali na mashine hizo, walifika pia na vifaa mbalimbali vya mahitaji ya wagonjwa, hususan watoto.

“Pamoja na mashine, tumetoa pia nepi za watoto na wakubwa, mafuta ya mwili, sabuni ya kuogea, sukari pamoja na virutubisho vya asidi ya foliki. Tunafahamu wagonjwa wana mahitaji mbalimbali, hivyo msaada huu ni sehemu ya kugusana nao,” alisema Bw. Ngonyani.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii MOI, Bi. Theresia Tarimo, alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wazazi na jamii juu ya umuhimu wa mama mjamzito kuhudhuria kliniki mapema ili kufahamu hali ya mtoto kabla ya kujifungua.

About the Author

You may also like these