Spika zungu afurahishwa na kambi maalum ya ugawaji wa miguu bandia bure

Na Amani Nsello-SWAMI

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu ametembelea kambi ya utoaji viungo bandia na kufurahishwa na hatua hiyo ambayo ni miongoni mwa njia bora za kugusa maisha ya Watanzania wanaoishi na ulemavu wa viungo.

Akizungumza leo Jumatatu Disemba 08, 2025 eneo la Swami Vivekanand Cultural Centre (SVCC), Masaki Jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kambi hiyo, Mhe. Zungu amesema hatua ya wataalamu wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kujengewa uwezo wa kutengeneza miguu bandia ni muhimu kwa ustawi wa huduma jumuishi nchini Tanzania.

“Tunataka zoezi hili liwe endelevu, pindi wataalamu wetu wa ndani watakapokuwa wamejengewa uwezo kamili, miguu bandia iwe inapatikana kwa bei nafuu… Chini ya laki tano, badala ya zaidi ya milioni mbili na nusu kama ilivyo sasa” amesema Mhe. Zungu

Wakati huo huo, Mhe. Zungu ameushukuru pia Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kuchangia uanzishwaji na utekelezaji wa kambi hiyo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo umeleta faraja kwa Watanzania wengi.

Kwa upande wake, Lakshay Anandi, Afisa Mawasiliano na Siasa wa Ubalozi wa India nchini Tanzania, amesema serikali ya India itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya afya na kubadilishana utaalamu.

Naye, Mtaalamu wa Vifaa Tiba na Viungo Saidizi (Bandia) kutoka MOI, Bw. Charles Mahua, amesema mpaka sasa jumla ya wahitaji 178 tayari wameshapatiwa viungo bandia kupitia kambi hiyo huku waliosajiliwa ni zaidi ya 1000.

About the Author

You may also like these