sisi sote ni sawa wafariji watoto waliolazwa MOI

Na Erick Dilli- MOI

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Sisi Sote ni Sawa imetoa msaada wa vitu mbalinbali kwa watoto waliolazwa kwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo na Muhimbili (MOI).

Akizungumza Agosti 13, 2025, katika hafla hiyo, mjumbe wa taasisi hiyo, Bi. Florence Mtegoa ‘Mama Kanumba’, amesema kuwa lengo la ziara yao ni kuwapa faraja na tabasamu watoto wanaoendelea kupata matibabu hospitalini hapo.

“Sisi kwa umoja wetu tumeona ni vyema kuja kuwafariji watoto hawa wanaopata matibabu hapa MOI. Tunatambua uhitaji ni mkubwa, lakini kwa kile kidogo tulichonacho, tumekuja kuwapa furaha na kuwatia moyo,” amesema Bi. Florence.

Kwa upande wake, Bw. Nathan Gilbert, Mratibu wa kikundi hicho, alibainisha kuwa wamekabidhi msaada wa sabuni ya unga na za kuogea, dawa ya meno, miswaki, nepi za watoto na maziwa, ili kusaidia mahitaji ya watoto waliolazwa.

Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa MOI, Bi. Sophia Nasson, aliwashukuru wanachama wa kikundi hicho kwa moyo wa upendo waliouonesha. Alisisitiza kuwa msaada huo unatoa faraja kubwa kwa watoto na familia zao, na kuwataka wadau wengine kuendelea kujitokeza kusaidia.

“Tunawashukuru sana kwa moyo huu wa kujali. Tunawaomba wadau wengine nao wajitokeze ili kuendeleza faraja kwa watoto hawa wakati wakiendelea na matibabu,” amesema Bi. Sophia.

About the Author

You may also like these