Na Erick Dilli- MOI
Kampuni ya Shelys Pharmaceuticals, ambayo ipo chini ya kampuni mama Aspen, imetoa jumla ya vitanda 10 vya wodini vyenye thamani ya shilingi 6,225,000 kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), kama sehemu ya mpango wake wa kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR).
Hafla ya makabidhiano ilifanyika leo, Oktoba 4, 2025 MOI, ikihudhuriwa na viongozi kutoka Shelys na uongozi wa taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Mauzo wa Aspen kwa Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Muhul Jotaniya, alisema lengo la kutoa vitanda hivyo ni kuchangia maendeleo ya sekta ya afya nchini.
“Kupitia utaratibu wetu wa kurudisha kwa jamii baada ya kupata faida ya biashara, tumeamua kuunga mkono jitihada za MOI kwa kukabidhi vitanda hivi 10, tukitambua mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma bora za afya nchini,” alisema Bw. Jotaniya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Bw. Fidelis Minja, akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, aliishukuru kampuni ya Shelys kwa mchango huo na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Tunatambua na kuthamini mchango huu muhimu kutoka Shelys. Utaongeza ufanisi katika kutoa huduma zetu na kuboresha mazingira ya wagonjwa wetu,” alisema Bw. Minja.
Aidha, mmoja wa wagonjwa wanaopata matibabu katika MOI, Bw. Christopher Thomas, alitoa shukrani zake kwa kampuni hiyo na kupongeza huduma bora anazopata katika taasisi hiyo.
“Nashukuru Shelys kwa kujali jamii. Mimi ni mgonjwa wa mgongo na mpaka sasa huduma ninazopata hapa MOI ni nzuri sana nawashukuru sana watoa huduma wote, amesema Bw. Thomas.