Na Amani Nsello- MOI
Ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamekumbushwa kutolipia huduma za matibabu kwa pesa taslimu (cash), badala yake walipie kupitia mifumo rasmi ya malipo ya serikali (Control number) ili kuepuka kutapeliwa.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Machi 21, 2025 na Muuguzi Mwandamizi, Bupe Ngunule kutoka Kitengo cha Udhibiti Ubora cha MOI wakati akijibu hoja na maoni kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo.
Bi. Bupe amesema kuwa bila kujali ndugu wa mgonjwa amekutana na mtumishi wa MOI amevaa sare za taasisi hiyo, hatakiwi kumpa pesa mkononi, na badala yake aombe ‘control number’ na kupewa risiti baada ya kufanya malipo.
“Haijalishi umekutana na mtumishi wetu (MOI) amevaa sare, haitakiwi kumpa pesa mkononi (cash), tuna mifumo rasmi ya kuchangia matibabu, hata baada ya kufanya malipo ni haki yako kudai risiti, hiyo itasaidia kuepukana na utapeli” amesema Bi. Bupe
Aidha, Bi Bupe ametoa elimu kwa ndugu hao wa wagonjwa namna ya kujikinga na ugonjwa wa M-Pox ikiwemo kunawa maji safi tiririka na kuepuka kushikana mikono.
Kwa upande wake, ndugu wa mgonjwa kutoka mkoani Kilimanjaro, Gladson Ngoda ameipongeza MOI kwa mandhari safi katika sehemu ya kusubiria huduma na wodini.