MOI yazindua mfumo mpya wa kuweka miadi kwa madaktari (MOI online appointment system)

Na Matha Kimaro-MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), imezindua rasmi mfumo mpya wa kuweka miadi na madaktari wa taasisi hiyo ujulikanao kama “MOI Online appointment system “ ambao humsaidia mgonjwa kuweka miadi ya kuonana na daktari anayemtaka, muda na klinki kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika MOI.

Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba, 15, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ambaye amesema lengo kuu la uanzishwaji wa mfumo huo ni kuwaondolea usumbufu na msongamano wa wagonjwa wanaofika kuweka miadi ya kuonana na daktari.

“Kupitia mfumo huu, mgonjwa ataweza kumchagua daktari anayemtaka, siku na muda wa kumuona na kliniki anayohitaji, utaondoa usumbufu wa wagonjwa kufika kliniki na kisha kuambiwa hiyo kliniki kwa leo haipo au daktari husika ana udhuru…wagonjwa hawatalazimika kufika mapema kwa ajili ya kuweka foleni ya kumuona daktari” amesema Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa

“Mgonjwa baada ya kufanya miadi atapokea ujumbe mfupi wa simu ukimtaarifu kukubalika kwa miadi yake, na hata pale daktari husika atakapopata udhuru mteja atapata taarifa kwenye simu yake na kumwezesha kuchagua daktari mwingine au amsubirie kwa siku nyingine”

Amesema mfumo huo mpya unapatikana saa 24/7 kwa kutumia simu janja, laptop au kishikwambi kupitia tovuti kuu ya taasisi https://www.moi.ac.tz au kiunganishi https://miadi.moi.ac.tz/appointment/ ambapo mgonjwa atalazimika kujaza taarifa zake fupi na kisha kuwasilisha.

“Tumejipanga kutoa huduma bora kwa kwa kuokoa muda wa mgonjwa kusubiri kumuona daktari, hii haina maana wagonjwa ambao hawajaweka miadi kwa mfumo huu hawatahudumiwa kwa wakati…wagonjwa wote watapata huduma kama kawaida isipokuwa mfumo huu mpya unampa uhakika wa mgonjwa kupata huduma kwa wakati na uhakika wa kuchagua daktari anayemtaka” amefafanua Dkt. Mpoki

Ametoa wito kwa Watanzania kuanza kutumia mfumo huo kwa ajili ya kuweka miadi kwa madaktari wa taasisi ya MOI ili kufanikisha adhima ya kutoa huduma za kidigitali katika kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

About the Author

You may also like these