Na Abdallah Nassoro-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewatunuku cheti cha udaktari bobezi wa matibabu ya kiuno na nyonga madaktari bingwa wawili baada ya kuhitimu mafunzo maluum (fellowship) ya miaka miwili katika fani hiyo.
Hafla ya madaktari hao kuhitimu na kutunukiwa vyeti hivyo imefanyika leo Oktoba, 24, 2025 katika taasisi ya MOI ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe: Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya alihudhuria.
Akiwatunuku vyeti hivyo Dkt. Mpoki amesema ni fahari kwa MOI kuendelea kuwa kituo mahiri cha mafunzo ya ubobezi ndani ya Afrika Mshariki na Kati na kwamba dhamira iliyopo ni kuwa kituo cha umahiri barani Afrika.
“Nawapongeza madaktari wabobezi mnaohitimu leo, hili ni jambo la kujivunia kwa taaisis yetu kuwa kituo mahiri cha ubobevu…kuhitimu kwenu leo kunaenda kuboresha hali ya utoaji huduma hapa MOI na katika eneo la Maziwa Makuu” amesema Dkt. Mpoki na kusisitiza kuwa
“Program kama hizi ziwe endelevu kwa maslahi ya taasisi, lakini pia kwa Taifa, madaktari wanasomea ubingwa na ubobevu katika fani ya mifupa, chaguo lao la kwanza liwe MOI kutokana na umahiri wetu katika kufundisha”
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Daktari Bingwa Bobezi wa Mifupa Dkt. Joseph Mwanga amesema program hiyo ya mafunzo ya ubobevu wa matibabu ya kiuno na nyonga imedumu kwa miaka mitano sasa ambapo leo hii mdaktari bingwa wawili wa MOI wamehitimu.
“Madaktari hao bingwa, ambao ni Dkt. John Nkinda na Dkt. Peter Mwandiga wamehitimu mafunzo maalum ya ubobevu wa matibabu ya kiuno na nyonga na sasa rasmi wanakuwa madaktari bingwa bobezi. Kuhitimu kwao kunaongeza idadi ya madaktari bobezi wa fani hiyo kufikia Wanne hapa MOI” amsema Mwanga na kuongeza kuwa
“Tangu kuanza kwa ‘fellowship’ endelevu mwaka 2020 jumla ya wataalam wanne wamehitimu, wawili kutoka nje ya nchi (Zambia na Rwanda), wawili kutoka Tanzania na mmoja kutoka Ghana yupo mbioni kuhitimu”