MOI yasogeza huduma za kibingwa na kibobezi maonesho ya nanenane dodoma

Na Amani Nsello- DODOMA

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inaendelea kung’ara katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma kwa kutoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika banda lake, MOI inatoa huduma mbalimbali za kitaalamu zikiwemo ushauri wa kiafya, uchunguzi wa awali (screening) na elimu ya kinga kwa wananchi kuhusu magonjwa ya mifupa, ubongo, mishipa ya fahamu na uti wa mgongo zilizowavutia wananchi wengi wa Dodoma na mikoa ya jirani

Akizungumza katika maonesho hayo leo Jumamosi Agosti 02, 2025, Daktari wa ubongo na mishipa ya fahamu MOI, Dkt. Manase Ng’wenzi amesema ushiriki wa MOI kwenye maonesho ya Nanenane una lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kutoa elimu ya afya kwa jamii ili wajikinge na maradhi hayo.

“Tumekutana na wananchi wengi wanaohitaji msaada au maarifa kuhusu matatizo ya uti wa mgongo, ajali na athari zake kwa mfumo wa fahamu. Tunawapa huduma ya ushauri na kuwashauri kufika MOI kwa matibabu zaidi. Tunajivunia pia kuwapa elimu ya kinga, ili wasisubiri hadi wapate matatizo,” anesema Dkt. Manase

Miongoni mwa wananchi waliotembelea banda la MOI ni Bi. Zahara Said, mkazi wa Dodoma, ambaye alifika kutoa ushuhuda wa huduma za MOI kuhusu mtoto wake aliyewahi kuumia kwenye ajali ya pikipiki mwaka 2024.

“Kwa kweli MOI wamekuwa msaada mkubwa kwetu. Mtoto wangu alipelekwa MOI baada ya ajali na leo hii anatembea mwenyewe… Nilipowaona hapa nimesisimka sana, walitutunza kama familia. Nashukuru kuona huduma kama hizi zinaletwa mpaka huku kwetu Dodoma,” amesema Bi. Zahara

Maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025” yaliaanza jana Agosti 01, na yatafikia tamati Agosti 08, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.

About the Author

You may also like these