MOI yashiriki kongamano la vifaa na teknolojia saidizi

Na Stanley Mwalongo- Dar es Salaam

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeshiriki kwenye kongamano la vifaa na teknolojia saidizi liliondaliwa na Mashirika yasio ya kiserikali ya Rehab Health na Kyaro Assistive Tech ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya teknolojia saidizi duniani inayofanyika Juni 04 kila mwaka.

Kongamano hilo limefunguliwa leo Juni 11, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Anthony Assey katika ukumbi wa Ummy Mwalimu, Dar es Salaam ambaye alimuwakilisha Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya.

Dkt. Assey amesema lengo la kongamano hilo ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa vifaa na teknolojia saidizi na hitaji la dharura la kuboresha upatikanaji wake.

“Kongamano hili linaakisi maono na jitihada za pamoja ya dunia ya kuboresha upatikanaji wa vifaa na ubunifu katika teknolojia saidizi ambazo zinaweza kukidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu aina mbalimbali, na linakwenda sambamba na viwango vinavyohamasishwa na Siku ya Kimataifa ya Vifaa na Teknolojia Saidizi” amesema Dkt. Assey

Ameongeza kwa kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na waandaaji wa kongamano hilo kama wadau wa huduma za utengemao, vifaa na teknolojia saidizi kwa kushirikiana na kusaidia jitihada za Serikali katika kuongeza upatikanaji wa teknolojia saidizi nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Rehab Dkt. Remla Shirima amesema kupitia kongamano hilo wataelezea umuhimu wa vifaa tiba na vifaa saidizi katika Maisha ya kila siku na kuchochea hatua za kuboresha upatikanaji na ubunifu wa teknolojia saidizi hapa Tanzania.

Kongamano hilo linafanyika kwa siku moja lenye kauli mbiu isemayo “Fungua Maisha ya Kila Siku kwa Watu wenye Ulemavu”.

About the Author

You may also like these