MOI yapokea msaada wa endoscope kutoka cure international

Na Amani Nsello- MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepokea msaada wa darubini ya kisasa ‘endoscope’ ya upasuaji wa ubongo na mgongo kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Cure International Limited, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya katika taasisi hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea kifaa hicho Mei 19, 2025 katika ukumbi wa Premier Lounge MOI, Daktari bingwa na mbobezi wa upasuaji wa ubongo wa MOI, Dkt. Hamis Shabani alilishukuru shirika hilo kwa msaada huo muhimu unaotarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za upasuaji wa ubongo bila kufanyiwa upasuaji mkubwa.

“Endoscope ni kifaa (darubini) cha kisasa kinachotuwezesha kufanya uchunguzi wa ndani ya mwili hususani ubongo kwa usahihi mkubwa, bila madhara makubwa kwa mgonjwa. Kifaa hichi kitatumika kuturahisishia kazi kwa madaktari wetu na kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Dkt. Shabani

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Cure International Bi. Freshia Mduma alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo kusaidia taasisi za afya barani Afrika kuboresha miundombinu na teknolojia ya tiba.

“Tunaamini kuwa kwa kushirikiana na MOI tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya maelfu ya wagonjwa,” alisema mwakilishi huyo.

About the Author

You may also like these