MOI yampa tuzo Prof. Roger kutoka marekani kwa kutambua mchango wake

Na Amani Nsello- Dar es Salaam


Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imempa tuzo Daktari bingwa na mbobezi wa ubongo, Prof. Roger Hartl kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake mkubwa katika Taasisi hiyo kwa ushirikiano wake wa zaidi ya miaka 16.

Prof. Roger alikabidhiwa tuzo hiyo Jumatatu Machi 24, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati wa Kongamano la 11 maalum kwa wataalam wa ubongo katika Hotel ya Protea Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kumkabidhi tuzo hiyo, Dkt. Mpoki alisema kuwa MOI imeamua kumpa tuzo kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kuwajengea uwezo madaktari na wataalam wa Taasisi hiyo kwa zaidi ya miaka 16 sasa.

“Tumempa tuzo Prof. Roger kwa kutambua mchango wake mkubwa kwa taasisi yetu (MOI), amekuwa na sisi kwa ukaribu kwa zaidi ya miaka 16 sasa, ameshirikiana nasi katika kuwajengea uwezo wataalam wetu na kuwapa mbinu mbalimbali kwa kualika wahisani kutoka mataifa mengi duniani ambao wametupatia vifaa tiba”- amesema Dkt. Mpoki

Aidha, Dkt. Mpoki amesema kuwa Taasisi hiyo itaendelea kuwa kinara katika tasnia ya upasauji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwani ndiyo Taasisi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambayo inatoa huduma hizo kama Taasisi na sio kama idara au sehemu ndogo ya hospitali.

Kwa upande wake, Daktari bingwa na mbobezi, Prof. Roger Hartl kutoka Chuo kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani, ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kumpatia tuzo na kutambua mchango wake ambapo ameaihidi kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa wakati wote.

About the Author

You may also like these