Na Abdallah Nassoro- DODOMA
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imejipanga kuendela kutoa huduma bora za matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu huku watumishi wakiaswa kutoa huduma kwa kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa umma ili kufikia azima hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Septemba, 09,2025 na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Marina Njelekela wakati akifungua kikao cha pili cha baraza la Sita la wafanyakazi wa MOI kinachoendelea katika hoteli ya Rafiki jijini Dodoma.
Amesema pamoja na kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma, bado ni muhimu kusisitiza utoaji wa huduma unazingatia ubora na maadili ya kazi na kwamba watakaojaribu kukiuka watachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya, nilipopokea nafasi hii nilianza kupata ujumbe kutokana kwa wagonjwa, wengi walipongeza kwa huduma nzuri, lakini wapo wachache walitoa maoni hasi, na ni wajibu wetu kushughulikia hizi kasoro ili huduma zetu zizidi kuwa bora zaidi” amesema Dkt. Njelekela
Ameongeza kuwa “Wale watakaokiuka maadili ya utumishi wa umma, hatutakuwa na uvumilivu nao, ni kwasababu tunataka kutoka hapa tulipo…mjipange kuridhisha wagonjwa, mpatie huduma hadi aridhike na hiyo ndiyo namna ya kuifanya taasisi yetu izidi kuaminika”
Amesema baraza hilo ndiyo chombo muhimu cha kuunganisha watumishi na menejimenti kwa kuwasilisha, kuchambua na kuzipatia majibu changamoto zinazokwanza ufanisi sehemu ya ya kazi.
Awali, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kikao hicho kitatoa muelekeo mpya wa huduma kwa wananchi na ni daraja la kuondokana na ufanyaji kazi kwa mazoea.
“Baraza hili limekuja kuzika ufanyaji kazi kwa mazoea (business as usual), hili ndiyo ‘bunge’ la wafanyakazi wa MOI, tukitoka hapa tunakuwa na ari mpya ya ufanyaji kazi” amesema Dkt. Mpoki
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), tawi la MOI Bw. Privatus Masula amesema watumishi wanaomba utumike waraka mpya wa posho za watumishi, pamoja na malimbikizo ya posho ili kuongeza ari ya utendaji kazi ambapo Mweneykiti wa Baraza la wafanyakazi MOI amesema jambo hilo litatekelezwa pindi hali ya kifedha itakapoimarika .
Katika kikao hicho baraza lilifanya uzinduzi wa mkataba wa kuunda baraza la wafanyakazi kati ya menejimeti ya MOI na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE).