Na Amani Nsello- DODOMA
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imehitimisha ushiriki wake katika Maonesho ya wakulima ‘Nanenane 2025’ jijini Dodoma kwa kutoa huduma kwa wananchi 1,981.
Huduma zilizotolewa na MOI zilihusisha uchunguzi wa awali (Screening), ushauri wa kitaalamu kuhusu matatizo ya mifupa, ubongo, mishipa ya fahamu, uti wa mgongo, tiba lishe, kipimo cha Ultrasound, Fiziotherapia (mazoezi tiba) na elimu ya kujikinga dhidi ya maradhi hayo.
Akizungumza kuhusu huduma hizo leo Jumapili Agosti 10, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma Daktari wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI, Dkt. Manase Ng’wenzi, amesema wananchi walionekana na hamasa kubwa ya kujitokeza kupata huduma na elimu ya afya.
“Ushiriki wetu umeleta manufaa makubwa, tumewahudumia wananchi wengi kutoka mikoa mbalimbali waliotumia fursa hii kupata ushauri wa kitaalamu na huduma maalumu bila gharama. Tunafurahia kuona mwamko huu wa afya,” amesema Dkt. Manase
Kwa upande wake, mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo kutoka Iringa, Bi. Zainabu Mussa, ameishukuru MOI kwa kushiriki maonesho hayo na kutoa huduma karibu na wananchi.
“Huduma hizi kwa kweli zimetufikia kwa urahisi. Tumepata elimu na uchunguzi bila kufuata foleni ndefu hospitalini. Tunawashukuru MOI kwa kujitoa,” amesema Bi. Zainabu.
Awali, Maonesho hayo yalipangwa kuhitimishwa Agosti 08, 2025, lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliagiza yaendelee hadi leo Agosti 10, 2025 ili wananchi waendelee kunufaika na huduma na elimu zinazotolewa na wizara, taasisi, kampuni na mashirika mbalimbali ya umma na sekta binafsi.
Maonesho hayo yalichagizwa kwa kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.