Na Mwandishi Wetu -Lusaka, Zambia
Washiriki wa maonesho ya kimataifa ya 97 ya kilimo na biashara yanayofanyika Lusaka Zambia wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma za ushauri na maelezo kuhusu huduma za kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zinazotolewa na MOI.
Taasisi ya MOI inashiriki katika maonesho hayo ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kutangaza tiba utalii kupitia huduma ya wagonjwa maalum na wakimataifa inayopatikana MOI.
Daktari bingwa na mbobezi wa Mifupa MOI Dkt. Joseph Sabas amesema maonesho hayo yamekua na mafanikio makubwa kwani wananchi wengi wa Zambia wamevutiwa na tarifa na elimu waliyopata kuhusu huduma zetu za kibingwa na kibobezi za MOI.
“Imekua na heshma kubwa kwetu kama Taasisi kupata fursa ya kunadi huduma zetu za kibingwa na kibobezi za mifupa , ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, wananchi wengi wa waliofika kwenye banda letu wamefurahishwa na uwepo wa huduma za MOI katika ukanda huu pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa na teknolojia mambo leo” Alisema Dkt. Sabas
Dkt. Sabas amesema ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho hayo umeratibiwa na ubalozi wa Tanzania nchini Zambia chini ya Mhe. Balozi, Lt. Gen. Mathew Edward Mkingule ambaye pamoja na maafisa ubalozi ambao kwa pamoja wamefanya kazi kubwa kuifanya Tanzania iibuke mshindi wa pili katika maonesho hayo.
Awali Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema alitembelea banda la Tanzania na kupongeza ushiriki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye maonesho hayo na kufurahishwa na maelezo mazuri aliyopewa na Mhe. Balozi wa Tanzania nchini Zambia kuhusu huduma za kibingwa na kibobezi za JKCI, MOI, MZRH na huduma za usafirishaji na uchukuzi zinazotolewa na kampuni ya ndege Tanzania na Mamlaka ya bandari Tanzania.