MOI yaadhimisha siku ya mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa kuendesha kliniki ya uchunguzi bure

Na Abdallah Nassoro-MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) leo Oktoba 25, 2025 imeadhimisha siku ya mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi Duniani kwa kufanya uchunguzi, kukata keki na kula pamoja na watoto wenye changamoto hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Daktari bingwa bobezi wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Dkt. Hamisi Shabani amewashukuru wadau wote wanaochangia matibabu ya watoto hao na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza.

“Tunawashukuru wadau wote wanaochangia matibabu ya watoto hawa wakiongozwa na MO Dewji Foundation, matibabu ya watoto hawa ni mchakato mrefu unahitaji subira na rasilimali fedha, hivyo uwepo wa wadau wanaochangia matibabu haya ni jambo la faraja kwa watoto na walezi” amesema Dkt. Shabani

Ameongeza kuwa “MOI ilianzisha kliniki ya mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi mwaka 2005, na kwa wakati huo tulikuwa unawafanyia upasuaji watoto 200 kwa mwaka na sasa tunawafanyia upasuaji watoto 800 kwa mwaka na zaidi ya 2000 wanahudhuria kliniki”

Dkt. Shabani ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kusaidia matibabu ya watoto hao ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya malezi ya watoto hao yameachwa mikononi mwa wanawake ambao kipato chao ni cha chini.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Sophia Nashon amewataka wazazi na walezi wa watoto hao kuendelea kuwa mstari wa mbele kusimamia matibabu yao ili kuendelea kupanda mbegu ya faraja kwao.

About the Author

You may also like these