Na Stanley Mwalongo- CHATO
Madaktari bingwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka hospitali ya rufaa ya kanda Chato kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kibingwa na kibobezi wa mifupa kwa wagonjwa Chato.
Upasuaji huo umefanyika Novemba 5, 2024 kupitia kambi maalum ya matibabu ya kibingwa na kibobezi ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu iliyoanza jana Novemba 4 mpaka 15 2024 katika hospitali ya rufaa ya kanda Chato.
Daktari bingwa na mbobezi wa mifupa Dkt. Bryson Mcharo amesema Taasisi ya MOI imesogeza huduma zake za kibingwa na kibobezi wilayani Chato ambapo leo wamefanikiwa kufanya upasuaji wa mifupa kwa wagonjwa wawili katika hospitali hiyo ya kanda.
“Leo hii kwa mara ya kwanza tumefanya upasuaji wa kibingwa na kibobezi wa mifupa kwa wagonjwa waliovunjika mifupa, mmoja mtoto alivunjika sehemu mbili mkononi (sehemu ya kiwiko na juu kidogo ya mkono) na mwingine alivunjika mifupa wa mguu wa kulia, tunatarajia baada ya muda wa wiki tatu watakuwa wameshapona“ amesema Dkt. Mcharo
Ameongeza kwa kusema kambi hii ni utekelezaji wa Agizo la Serikali ya Awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na ametoa wito kwa wakazi wote wa kanda ya ziwa; Mwanza, Bukoba, Geita na mikoa ya jirani kufika hospitali ya rufaa ya kanda Chato ili kupata huduma hizo.
Kwa upande wake Daktari wa upasuaji wa mifupa hospitali ya kanda ya rufaa Chato Dkt. Raymond Richard amesema ni mara ya kwanza kufanya upasuaji huo ambapo mwanzo wagonjwa kama hao walikuwa wanapewa rufaa ya kwenda MOI, Dar es Salaam lakini sasa watakuwa wanafanyiwa upasuaji wilayani Chato.