Na Amani Nsello- MBAGALA
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Umoja wa Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Wa Adiventista Wasabato Tanzania (ATAPE) wametoa matibabu ya kibingwa na kibobezi bure katika kambi maalum kwa wakazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kambi hiyo Mei 12, 2025 katika Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala, Daktari Bingwa na Mbobezi wa Mifupa wa MOI Dkt. Allen Kisanga alisema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa na kibobezi kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali ya awamu ya sita.
“Katika kutekeleza agizo la serikali hii ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi kwa wananchi ndiyo maana tumekuja hapa Mbagala, ili sasa wakazi wa Mbagala waje hapa Dar Live wapatiwe huduma hizo badala ya kuzifuata MOI” alisema Dkt. Kisanga
Aidha, Dkt. Kisanga alitoa rai kwa wakazi wa Mbagala na viunga vyake kutumia fursa hiyo adhimu kujitokeza kwa wingi kupata matibabu ya kibingwa na kibobezi kutoka kwa wataalam hao wa MOI.
Kwa upande wake, Mratibu wa kambi hiyo kutoka ATAPE, Dkt. Samweli Kikaro aliishukuru Taasisi ya MOI kwa kupeleka wataalam wake katika kambi hiyo na kuwapatia matibabu ya kibingwa na kibobezi kwa wakazi wa Mbagala.
Kambi hiyo ilianza Mei 11, 2025 na itafikia tamati Mei 17, 2025 Dar Live, Mbagala Jijini Dar es Salaam.