MOI kuwajengea uwezo madaktari pemba kutoa huduma za msingi za mifupa na ubongo

Na Abdallah Nassoro-Pemba

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeombwa kuwajengea uwezo madaktari wa kisiwani Pemba, Zanzibar ili waweze kutoa huduma za msingi za matibabu ya mifupa na ubongo yanayosababishwa na ajali.

Ombi hilo limetolewa leo Julai, 24, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Khamis Abdulla Said katika ufunguzi wa maonesho ya elimu ya juu yanayoendelea katika viwanja vya Gombani Pemba.

Amesema visiwa vya Pemba kama maeneo mengine ya nchi yanakabiliwa na ajali za barabarani na kwamba imekuwa ni vigumu kwa watalaam kutoa huduma za msingi ili kumuimarisha mgonjwa kabla ya kumpa rufaa ya kwenda hospitali kubwa kutokana na kukosa ujuzi wa kutosha kufanya hivyo.

“Mnajua changamoto ya usafiri iliyopo hapa Pemba, bodaboda akipata ajali inakuwa vigumu kumpatia huduma ya msingi kwenye matibabu ya mifupa na ubongo, niwaombe na mpeleke salamu kwa mkurugenzi wetu kuwa tunaomba muwajengee uwezo madaktari wa Pemba” amesema mhe. Said na kuongeza kuwa

“Mmekuwa mkifika Unguja, lakini kwa huku Pemba ni mara ya kwanza, nawapongeza sana, sasa nyinyi ndiyo kituo cha umahiri kwenye matibabu haya ni lazima muwe na mpango wa kuwasaidia watalaam wa hapa ili majeruhi wa huku wapate huduma bora.

Awali Dkt. Catherine Hance wa MOI, amemweleza Katibu Mkuu huyo kuwa lengo la MOI kushiriki katika maonesho hayo ni kutoa elimu na huduma ya ushauri kwa wananchi.

“Sisi MOI tunatoa huduma za kibingwa na kibobezi za Mifupa, Mgongo na Mishipa ya Fahamu na ili kuhahilisha huduma zinawafikia wananchi wengi tunayo program ya Tiba mkoba ambapo pia tunawajengea uwezo watalaam katika eneo husika ili waweze kutoa huduma hizo” amesema Dkt. Catherine

About the Author

You may also like these