MOI kusaini makubaliano ya kutibu wagonjwa na kuwajengea uwezo madaktari comoro

Na Mwandishi Wetu- COMORO (Anjouan)

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kutia saini ya makubaliano ya kutoa matibabu ya kibingwa ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa wananchi na kuwajengea uwezo madaktari wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro.

Hayo yalibainishwa jana Septemba, 04, 2025 na Gavana wa kisiwa hicho Dkt. Youssef Zaidou wakati wa ufunguzi wa kambi maalum ya matibabu ya madaktari kutoka Tanzania ambapo amesema ni faraja kwa wakazi wa kisiwa hicho kupata fursa ya kutibiwa na madaktari bingwa kutoka Tanzania.

Amesema wakazi wa kisiwa hicho wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za matibabu ya kibingwa na kwamba kuingia kwa makubaliano hayo itasaidia kuwajengea uwezo madaktari wazawa na kuinua sekta ya afya katika kisiwa hicho.

“Idadi kubwa ya wananchi wa hapa Anjouan wanakwenda Tanzania kwa matibabu, lakini kwa bahati mbaya huishia kwenye hospitali ambazo hazina wataalam wabobezi hivyo matibabu yao hayakamiliki, lakini leo hapa tunafungua ukurasa mpya wa njia bora ya wananchi wetu kuja kutibiwa huku wakipewa hadhi tofauti” alisema Dkt. Zaidou

Aliongeza kuwa “Sisi wana Anjouan tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Julai, 6, mwaka huu (2025) wakati sherehe za uhuru wa Comoro”

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu alisema, wataalam hao 52 kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) waliogawanyika katika kada 12 watatoa matibabu bure kuanzia tarehe 5 hadi 11 Oktoba 2025 kwa wakazi wa visiwa vya Anjouan,

“Kambi hii maalum ya matibabu ni kielelezo cha uhusiano mzuri baina ya nchi hizi mbili uliosimikwa katika mzizi ya undugu na mshikamano…kwa namna ya kipekee hatunabudi kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukuza uchumi wa diplomasia”

Kaimu Mwenyekiti wa Tiba Utalii wa MOI, Dkt. Joseph Sabas alisema makubaliano hayo yatawezesha wagonjwa kutoka visiwa hivyo kupewa tufaa kwenda na kupatiwa matibabu kwa urahisi zaidi, sambamba na kuwajengea uwezo madaktari.

“MOI ipo tayari kuendeleza ushirikiano wa kutoa kutoa matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa Anjouan, lakini pia kuwajengea uwezo madaktari wa hapa waweze kutoa huduma za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu” alisema Dkt. Sabas

About the Author

You may also like these