Na Mwandishi Wetu-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeungana na taasisi zingine za JKCI, MNH ,ORCI na hospitali ya Benjamin Mkapa katika Kambi maalum ya matibabu katika visiwa vya Anjouan nchini Comoro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Kaimu Mwenyekiti wa Tiba Utalii MOI Dkt. Joseph Sabas amesema ushiriki wa MOI katika Kambi hiyo unalenga kukuza Tiba Utalii nchini.
“Sisi Madaktari bingwa wa Mifupa na Ubongo kutoka MOI, tumeungana na wenzetu kama taifa kwenda kutoa matibabu kwa wananchi wa visiwa vya Anjouan nchini Comoro na tupo tayari kuwahudumia” amesema Dkt. Sabas
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tiba Utalii nchini, Dkt. Peter Kisenge amesema Kambi hiyo inahusisha madaktari bingwa kutoka MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma.
“Kambi hii pia ni utekelezaji wa aahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa sherehe za uhuru wa Comoro akiwa mgeni rasmi” amesema Dkt. Kisenge
Ameongeza kuwa “Rais aliahidi kuendeleza ushirikiano katika sekta ya afya na sisi tunaenda kutoa matibabu kwa wananchi wa visiwa hivyo ikiwa ni awamu ya pili⦠Ushirikiano huu utakuza pia Tiba Utalii nchini”