Na Abdallah Nassoro-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inautaarifu umma kuwa itaendesha zoezi la uchunguzi, elimu na ushauri wa magonjwa yasiyoambukiza kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza Duniani ambayo hufanyika kila wiki ya pili ya mwezi Novemba.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe: Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akiongea na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba, 7, 2025 na kufafanua kuwa uchunguzi huo utafanywa na madaktari bingwa na bobezi kutoka MOI katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia Jumatatu tarehe 10 mpaka Jumamosi tarehe 15 Novemba 2025, saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
“Huduma zitakazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa awali, ushauri na elimu kwa magonjwa ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kiharusi. Pia kutakuwa na huduma za mazoezi tiba (Fiziotherapia) pamoja na ushauri wa tiba lishe “ amesema Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa
“Huduma hizo zitatolewa bure kwa wagonjwa wasio na bima ya afya, na kwa wale wenye bima ya afya, bima zao zitatumika kupata huduma hizo ili kurahisisha muendelezo wa matibabu iwapo mgonjwa atatakiwa kufanya hivyo”
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa kitengo cha magonjwa ya ndani na dawa, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani Dkt. Deodata Matiko ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima afya zao ili wajue afya zao, kupata matibabu na kujikinga na magonjwa hayo.