Na Stanley Mwalongo- HANDENI
Akiwa kwenye ziara wilayani Handeni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Februari 23, 2025 aliagiza kwamba hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ianze kutoa huduma za matibabu ya upasuaji wa mifupa na majeruhi.
Katika kutekeleza maagizo hayo wataalam kutoka Taasisi ya MOI wamefika hospitali hiyo Februari 25, 2025 ili kufanya tathimini ya miundombinu na vifaa tiba vilivyopo katika hospitali hiyo ili kuanza kutoa huduma hizo.
Ujio wa wataalam hao Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI ) pia ulikuwa na lengo la kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Handeni katika kutoa huduma hizo.
Akizungumzia ziara ya wataalam hao kutoka Taasisi ya MOI Mkurugenzi wa huduma za upasuaji wa mifupa- MOI Dkt. Anthony Assey amesema wameridhishwa na miundombinu na vifaa tiba vilivyopo katika hospitali hiyo ya wilaya ya Handeni na kwamba vitarahisisha utoaji wa huduma hizo za mifupa na majeruhi.
“Sisi kama Taasisi ya MOI tutaleta timu ya wataalam pamoja na vifaa vya upasuaji kama vipandikizi pamoja na vitu vingine kwaajili ya kutibu wagonjwa na tunategemea matibabu haya yataanza muda si mrefu baada ya maandalizi ya mwisho kufanyika kati ya hospitali hii na MOI kama ambavyo tumeelekezwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama (Mb)” amesema Dkt. Anthony
Dkt. Anthony amesema lengo la kufanya ziara katika hospitali hiyo ya Handeni ni kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuilea na kuijengea uwezo hospitali hiyo ili iweze kutoa huduma za matibabu ya mifupa, migongo na mivunjiko.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni Saitoti Steven ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kufika mapema kufanya tathimini katika hospitali hiyo ili huduma za kibingwa za matibabu ya mifupa zianze kutolewa kwa wananchi, kwani serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vifaa tiba katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Handeni Dkt. Kisaka Kachua amesema awali wagonjwa wa mifupa na majeruhi walilazimika kuwapa rufaa za kwenda Taasisi ya MOI kwaajili ya matibabu lakini kuanzisha kwa huduma hizo zitapunguza gharama na adha kwa wananchi kwa kuwasogezea huduma hizo karibu yao.