Na Abdallah Nassoro-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya ya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zimekubaliana kuweka kambi ya matibabu Jamhuri ya Watu wa Comoro ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kukuza tiba utalii nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Comoro Mhe: Youssoufa Mohamed Ali ambaye amefanya kikao na viongozi wa taasisi hizo siku ya Jumatatu Oktoba 4, 2024 katika ukumbi wa Taasisi ya JKCI.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mhandisi Ismail Rumatila aliyeongoza ujumbe huo amesema Tanzania ilitiliana saini ya ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa Comoro Julai, 2024 katika sekta ya afya ulioruhusu uhamishaji wa wagonjwa kutoka Comoro na kuletwa katika hospitali za afya za umma za Tanzania kwa matibabu.
“Kupitia ushirikiano huu taaisi zetu za MOI, JKCI na MNH watalazimika kwenda Comoro na kuona namna bora ya kutoa matibabu kwa wananchi na kuwajengea uwezo watoa huduma wa Comoro…hatua hii niutekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka Tanzania iwe kituo cha umahiri wa tiba utalii barani Afrika” amesema Mhandisi Rumatila
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Comoro Mhe: Yuossoufa Mohamed Ali amesema ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro ni wa kihistoria kuaniza mwaka 2003 na kwamba zaidi ya raia 2000 wa Comoro huingia nchini Tanzania kwa mwezi na asilimia 70 ni kwa ajili ya matibabu.
“Tanzania inapata dolla za kimarekani 100 millioni kutoka Comoro, hii inaonesha ushirikiano wetu ni wa umuhimu…nichukue fursa hii kuwaomba mfike Comoro ili muone namna ambavyo munaweza kutusaidia kuwatibiatibu wananchi wetu, pia kuwajengea uwezo wataalam wetu” amesema Mhe Ali