Na Erick Dilli- Geita
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari amepongeza jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika utoaji huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Septemba 24, 2025 wakati Dkt. Sukari alipotembelea banda la MOI kwenye Maonesho ya Nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini katika viwanja vya nanenane Geita na kufurahishwa kwa jitihada kubwa zinazofanywa na MOI nchini.
“Tunashukuru na tunatambua juhudi ya Taasisi (MOI) katika utoaji huduma katika Taifa letu kwenye Maswala ya Mifupa, ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu na kuweza fanikiwa kumaliza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata matibabu haya, kwa hilo hongereni sana” amesema Dkt Omari
Kwa upande wake Daktari kutoka kitengo cha Mifupa MOI, Dkt. Rahma Magina amemuelezea Mganga Mkuu huyo hatua ambayo MOI imefikia kwa upande wa teknolojia kwenye kuhudumia wagonjwa mbalimbali.
“Taasisi imeona kunakuwa na msongamano ya wagonjwa hospitalini na kupelekea kukaa mda mrefu kusubiria huduma hivyo tumeanzisha mfumo wa kuweka miadi ya kumuona Daktari kwa njia ya mtandao (Online Appointment system) ukiwa sehemu yoyote nchini na kupelekea mgonjwa kufika muda ambao amechagua wa kuja kumuona daktari anayemtaka” amesema Dkt. Rahma
Taasisi ya MOI inashiriki katika maonesho ya nane ya kimataifa ya teknolojia ya madini hapa geita mpka septemba 28, 2025 kutoa ushauri wa huduma za kibingwa na kibobezi za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu kwa wakazi wa mikoa ya geita na mikoa jirani.