Na Amani Nsello- MOI
Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepatiwa mafunzo ya utekelezaji bora wa bajeti ya maendeleo ya Taasisi hiyo ya mwaka wa fedha 2025/26 ili kuendelea kuboresha huduma kufikia dira ya taifa ya 2050.
Hayo yalibainishwa Agosti 26, 2025 na Meneja Mipango, Ufuatiliji & Tathimini wa MOI, Bw. Elisha James Sibale wakati wa mafunzo ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa wajumbe wa menejimenti ya MOI.
Bw. Sibale alisema taasisi imejipanga kuhakikisha rasilimali zilizotengwa zinatumika kwa ufanisi mkubwa
“Bajeti ya MOI kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imejikita katika uwekezaji wa huduma za kibingwa, tafiti na matumizi ya teknolojia ya kisasa. Hatua hii inalenga kuhakikisha tunachangia moja kwa moja kufikia azma ya Taifa iliyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa miaka mitano pamoja na kujipanga vema kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kupitia Mpango na Bajeti utakao andaliwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027” alisema Bw. Sibale
Kwa upande wake, Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Bw.Mintanga Milulu, alisema kuwa wizara itaendelea kusimamia na kuhakikisha taasisi za afya zinatekeleza bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa.
“MOI ni moja ya nguzo muhimu katika sekta ya afya, hivyo utekelezaji wake wa mpango na bajeti lazima uendane na dira ya taifa. Wizara itaendelea kutoa usimamizi wa karibu na msaada wa kitaalamu,” alisema Bw. Milulu
Aidha, Mtakwimu Mkuu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bi. Mary Mshangila, alisema kwamba serikali imeweka mkazo kwenye matumizi sahihi ya fedha za umma, kuhakikisha taasisi zinabaki na uendelevu wa kifedha
“Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kuhakikisha taasisi kama MOI zinapata usimamizi bora wa kifedha. Tunataka kila shilingi inayotolewa ichangie moja kwa moja katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa ifikapo mwaka 2050,” alisema Bi. Mary