Na Amani Nsello- MOI
Mashabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Simba SC tawi la Goba lijulikanalo kama ‘Simba Makini’ wametoa msaada wa vitu mbalimbali na kuwajulia hali watoto wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Mashabiki hao wametoa msaada huo leo Ijumaa Machi 21, 2025 katika wodi namba 5 MOI ambapo Katibu wa tawi hilo, Neema David Shingo amesema kuwa wameamua kutoa msaada kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa ajili ya kufanya matendo ya huruma na kuwajulia hali watoto hao.
“Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani tumeguswa tukaamua kuja hapa (MOI) kufanya matendo ya huruma na kuwajulia hali watoto hawa, tulichangishana na tukapata tulichojaaliwa”-amesema Bi. Neema
Bi. Neema amesema kuwa wamechangia fedha kwa ajili ya kuchangia matibabu ya mtoto mmoja na pia wametoa taulo za kike, sabuni, mafuta,dawa za meno na pampasi.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa MOI, Teofrida Mbilinyi amewashukuru mashabiki hao kwa masada wao na kuwaomba waeendelee kuwa na moyo huo wa kutoa.