Makamu wa Rais Dkt. Mpango aagiza MOI kushirikiana na wadau wengine kudhibiti ajali za barabarani

Na Abdallah Nassoro – MBEYA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Watanzani Dkt. Philip Mpango ameiagiza Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kushirikiana na jeshi la polisi, vyombo vya habari pamoja na wadau wengine kutoa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri ili kupunguza ajali za barabarani.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo Ijumaa Februari 21, 2025 alipotembea banda la MOI katika mkutano wa 109 wa washitiri wa elimu kwa umma unaomalizika Leo katika ukumbi wa City Park Garden jijini Mbeya.

Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo MOI imeshiriki katika kutoa huduma za kibingwa za Mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa washitiri na wakazi wa mkoa wa Mbeya bila gharama yoyote.

“Hongereni sana kwa kazi kubwa manayoifanya, jambo hili linahitaji ushirikiano na wadau wengine kama vyombo vya habari kutoa elimu, ili kupunguza hizi ajali” amesema Dkt. Mpango na kuongeza kuwa

“Kuna wakati nilifika pale MOI nikakuta vijana wengi wanapata matibabu kutokana na ajali, munafanya nini kuwasaidia Hawa?”

Mapema Daktari Bingwa wa Mifupa wa MOI Dkt. Tumaini Minja amemueleza Makamu wa Rais Dkt. Mpango kuwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa matibabu ya kibigwa kwa majeruhi wa ajali na kunusuru maisha yao.

“Ili kuwawezesha watanzania wengi kupata huduma za kibingwa na kibobezi tumekuwa tukiendesha kliniki jongefu maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, pia tumewajengea uwezo na kupeleka huduma ya tiba mkoba katika hospitali za kanda Mtwara,hospitali ya Nyangao Lindi ,hospitali ya St. Benedict Ndanda, hospitali ya kanda Chato, hospitali ya Nkinga Tabora na hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzaibar ” amesema Dkt. Minja

Aidha Dkt. Minja amesema MOI imefanikiwa kutoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wagonjwa 540 wakati wa mkutano huo wa washitiri.

About the Author

You may also like these