Madaktari MOI na MNH

Dar es Salaam, 12/03/2019. Madaktari bingwa wa Upasuaji wa Ubongo ,Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI kwa kushirikiana na Madaktari bingwa wa Pua, Koo na Masikio wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye Ubongo kwa kupitia kwenye tundu la Pua (Endoscopic Trans nasal transsphenoidal pituitary surgery) ambao ulikua haufanyiki hapa nchini.

Upasuaji huo wa kihistoria umefanywa kwa mafanikio makubwa na jopo la madaktari bingwa wazalendo wanne kwa kutumia muda wa masaa matatu ambapo wamefanikiwa kuondoa uvimbe wote.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu MOI, Dkt Lemery Mchome amebainisha kwamba upasuaji huu umefanyika kwa mafanikio makubwa na mgonjwa hatatumia muda mwingi hospitalini na ataruhusiwa kwenda nyumbani ndani ya siku chache.

“Upasuaji huu ni wa kisasa na wenye matokeo chanya kwa mgonjwa kwani tunaondoa uvimbe kwa kupitia puani badala ya kufungua fuvu kama ambavyo imezoeleka ambapo mgonjwa anatumia muda mwingi kurudi kwenye hali ya kawaida, pia kwa njia hii mgonjwa hatahitaji kupumua kwa kutumia mashine baada ya upasuaji na tutamruhusu ndani ya siku chache zijazo” Alisema Dkt Lemery

Dkt Lemery amesema upasuaji huu umewezekana kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali katika miundombinu pamoja na wataalamu hivyo madaktari bingwa Wazalendo wanaweza kufanya upasuaji huo bila ya utegemezi wa wataalamu kutoka mataifa mengine.

Kwaupande wake daktari bingwa wa magonjwa ya Masikio, Pua na Koo Dkt Edwin Liyombo Kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema upasuaji huu wa kuondoa uvimbe kwa kupitia kwenye tundu la pua ni wa kisasa na wenye matokeo bora zaidi ya njia iliyozoeleka ya kufungua fuvu.

“Tumefanya upasuaji huu kwa mafanikio makubwa sana, tunaamini mgonjwa atakuwa salama na atakwenda nyumbani mapema, awali wagonjwa hawa walilazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa, kwakuwa vifaa vipo hapa MOI tumeamua tushirikiane kuwahudumia Watanzania wenzetu hapa nchini na kuipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa gharama kubwa” alisema Dkt Liyombo

 Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli umepelekea huduma nyingi za kibingwa ambazo zilikua hazipatikani hapa nchini kuanzishwa na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi.

About the Author

You may also like these