Madaktari bingwa wa mifupa 43 wanolewa mbinu mpya za kutibu mifupa iliyovunjika na madhara yatokanayo na ajali

Na Amani Nsello- Dar es Salaam

Jumla ya madaktari bingwa 43 wa mifupa kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Rwanda, Zambia na Zimbabwe wamepatiwa mafunzo ya kitaalam ya Teknolojia mpya na za kisasa za kutibu mifupa iliyovunjika.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa siku 3 na taasisi ya AO Alliance ya nchini Marekani kwa kushirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika hoteli ya Protea (Courtyard), jijini Dar es Salaam, yalihusisha mbinu mbalimbali za kibingwa na za kisasa katika matibabu ya mifupa iliyovunjika pamoja na madhara yatokanayo na ajali.

Hayo yamebainishwa Jumapili Agosti 24, 2025 na Mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Mifupa kutoka MOI Dkt. Joseph Mwanga, ambaye ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwajengea uwezo wa wataalam wa tiba ya mifupa barani Afrika ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na za viwango vya kimataifa.

“Kozi hii imelenga kuwajengea uwezo na kuwakumbusha madaktari bingwa katika kutumia njia sahihi zinazoheshimu baiolojia ya mfupa na tishu laini, huku zikihakikisha mgonjwa anapona haraka na kurejea katika shughuli zake za kila siku.” amesema Dkt. Mwanga

Kwa upande wake, mmoja wa wakufunzi wa kimataifa kutoka Marekani katika Taasisi ya AO Alliance Dkt. Coscia Michael , amesema mafunzo hayo ni ya kipekee kwani yanawaandaa madaktari bingwa wa Afrika kushiriki katika mabadiliko makubwa ya kitaalam duniani.

“Tunawapa madaktari hawa nyenzo mpya ili waendane na mabadiliko ya kimataifa katika tiba ya mifupa… Hii ni hatua muhimu ya kuboresha huduma za afya barani Afrika na kupunguza changamoto za muda mrefu za wagonjwa.” amesema Dkt. Michael

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameeleza namna walivyonufaika. Dkt. William Mgisha, Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa MOI, amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kupata uelewa wa mbinu za upasuaji usio na madhara makubwa kwa wagonjwa.

Mshiriki mwingine, Dkt. Kuzivakwesha Mbiriri kutoka Hospitali ya Parivenyatwa ya nchini Zimbabwe, amesema kwamba mafunzo hayo yatawezesha kuboresha huduma kwa majeruhi wa ajali za barabarani.

About the Author

You may also like these