Kwaheri Dkt. Mango, ‘Mtu wa watu’

Na Amani Nsello- UNUNIO

Mikono ya kwaheri, huzuni na majonzi vilitawala kutoka kwa waombelezaji katika makaburi ya kwa Kondo, Ununio jijini Dar ea Salaam walipousindikiza mwili wa marehemu Dkt. Mechris Mango, aliyekuwa Daktari Bingwa wa Radiolojia na Mkuu wa Idara ya Uchunguzi MOI katika nyumba yake ya milele.

Mazishi hayo yaliongozwa na Mganga Mkuu wa Seriakli, Dkt. Grace Magembe kwa niaba ya Wizara ya Afya, ambaye amesema kuwa sekta ya afya imepoteza mtu muhimu kwani ilikuwa bado ikimuhitaji kwakuwa alikuwa mwalimu kwa wengine.

“Kama wizara kutoka moyoni kabisa tumehuzunishwa sana na kifo cha Dkt. Mango, alikuwa bado tunamhitaji sana, alikuwa anaendelea kupanda mbegu (kufundisha wenzake)” amesema Dkt. Magembe

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa MOI, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kwamba Dkt. Mango hakuwa mbinafsi katika suala la maarifa, alikuwa msaada kwa wenzake hususani waliotaka kujifunza kuhusiana na taaluma ya Radiolojia

Watumishi wenzake walimuelezea Dkt. Mango kama mtu wa watu mnyenyekevu, mwenye moyo wa kusaidia na aliyejali ustawi wa kila mmoja.

“Alikuwa sio tu kiongozi, bali ni mshauri na rafiki… Wakati wowote ulikuwa na shida Dkt. Mango alikuwa mtu wa kwanza kukuuliza uko salama?” amesema Zaina Msangi, Mhudumu wa Afya MOI

Shughuli za mazishi zilianza nyumbani kwao marehemu Dkt. Mango, Kinondoni Mkwajuni, ambako waombolezaji walikusanyika kwa salam na maombi na kuendelea kumkumbuka kama mtu mwenye upendo na mchapakazi mahiri aliyetoa mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini Tanzania.

Ibada fupi ya faraja ilifanyika Kanisani SDA Magomeni, ambako Mchungaji Jeremiah Izungo aliongoza sala na kutoa mahubiri yaliyogusa mioyo ya waombolezaji, akisisitiza juu ya maisha ya huduma na upendo ambayo Dkt. Mango aliyaishi. Alisema alikuwa si tu daktari, bali pia kiongozi mwenye maono na mwelekeo wa kusaidia wengine kwa moyo wake wote.

About the Author

You may also like these