Kuelekea siku ya mtindio wa ubongo duniani, MOI yatoa matibabu bure kwa watoto wenye changamoto hiyo

Na Amani Nsello- Dar es Salaam

Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mtindio wa Ubongo Duniani yanayofanyika Oktoba 6 kila mwaka, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetoa huduma za matibabu bure kwa watoto wenye changamoto ya mtindio wa ubongo.

Huduma hizo zimetolewa leo Jumamosi Oktoba 04, 2025 katika viwanja vya shule ya Genesis iliyopo Msasani, jijini Dar es Salaam.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa kwa watoto MOI, Dkt. Bryson Mcharo, amesema huduma hiyo imelenga kuwafikia watoto wenye uhitaji maalum ambao mara nyingi wanakosa huduma hizo kutokana na gharama kubwa za matibabu.

“Tumeamua kuja moja kwa moja kwenye jamii ili kuwahudumia watoto hawa bure… Lengo letu ni kuongeza uelewa kuhusu mtindio wa ubongo na kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi sawa ya matibabu na uangalizi maalum wa kiafya,” amesema Dkt. Mcharo.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Theresia Tarimo, amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma za kijamii na ushauri kwa wazazi ili kusaidia watoto wanaoishi na changamoto hiyo kupata huduma bora zaidi.

“Huduma hizi hazihusiani tu na matibabu ya mwili, bali pia tunawapa wazazi ushauri na elimu ya namna ya kuwalea watoto wenye mtindio wa ubongo kwa upendo na uvumilivu,” amesema Bi. Lyimo.

Mmoja wa wazazi waliopata huduma hizo, Bi. Amina Juma, ameishukuru MOI kwa huduma hiyo, akisema imekuwa faraja kubwa kwa familia yake.

“Mtoto wangu amekuwa na changamoto ya mtindio wa ubongo tangu akiwa na miezi sita. Leo nimepata matibabu bure na maelekezo mazuri kutoka kwa madaktari wa MOI. Tunashukuru sana kwa moyo huu wa huruma,” amesema Bi. Amina.

Huduma hizo zimeendelea kuhamasisha jamii kutambua kuwa mtindio wa ubongo ni hali inayoweza kudhibitiwa kupitia matibabu, mazoezi ya viungo, na ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na wataalamu wa afya.

About the Author

You may also like these