Na Martha Kimaro- MOI
Familia ya Dkt. Abraham Muro wa Tegeta jijini Dar es Salaam imetoa tuzo ya pongezi kwa madaktari na wauguzi wanaohudumu katika wodi namba 4B ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), kama ishara ya shukrani kwa huduma bora walizozitoa kwa mama yao aliyekuwa akipatiwa matibabu katika taasisi hiyo.
Tukio hilo lilifanyika tarehe 18 Agosti 2025, ambapo Bi. Isabella Muro, kwa niaba ya familia, aliwashukuru viongozi na wataalamu wa wodi hiyo kwa kumhudumia kwa upendo mama yao Desphoria Muro aliyekuwa amelazwa katika wodi hiyo kwa matibabu.
“Katika kutambua huduma bora zinazotolewa na MOI, familia yetu imeona ni vyema kuwakabidhi cheti hiki cha pongezi kama shukrani kwa matibabu bora yaliyotolewa kwa mama yetu aliyekuwa na changamoto ya goti. Hakika moyo wenu wa kujituma umeacha alama njema katika familia yetu,” alisema Bi. Isabella.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kiongozi wa Wodi 4B MOI, Bi. Sada Mbilinyi, aliahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wote kama sehemu ya misingi ya taasisi hiyo.
“Kwa kushirikiana na uongozi na watumishi wenzangu, tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu na kuhakikisha wanarejea katika shughuli zao wakiwa na amani ya moyo,” alisema Bi. Mbilinyi.