Na Amani Nsello- MOI
Familia ya Bw. Jackson Paul Kehengu imetoa msaada wa vitimwendo (wheelchairs) 10 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya familia hiyo Agosti 16, 2025, Bw. Bw. Kehengu alisema msaada huo ni sehemu ya mchango wao wa kijamii wenye lengo la kuboresha ustawi wa wagonjwa na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya.
“Tumeamua kutoa msaada huu ili kusaidia wagonjwa wanaohitaji msaada wa kutembea waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi,” alisema Bw. Kehengu.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi wa MOI ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa taasisi hiyo, Dkt. Asha Abdulah, aliishukuru familia hiyo kwa moyo wa kujitolea na kusisitiza kuwa msaada huo utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuwahudumia wagonjwa.
“Tunathamini sana mchango huu, kwani vitimwendo hivi vitarahisisha kazi ya kuwahudumia wagonjwa, hususani wale wanaopata changamoto za kutembea,” alisema Dkt. Asha.
Pia, Dkt. Asha alitumia wasaa huo kuomba wadau wengine waendelee kujitokeza kutoa msaada wa hali na mali kwani mahitaji ni mengi katika taasisi hiyo